October 21, 2012

Kenya Yathibitisha Kushiriki CECAFA 2012 Uganda



Shirikisho la mchezo wa soka nchini Kenya, Football Kenya Federation (FKF) limethibitisha kuwa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars itashiriki katika michuano ya kuwania kombe la mataifa bingwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati-CECAFA ambayo imepangiwa kuanza tarehe ishirini na nne mwezi ujao hadi Desemba tarehe nane.
Harambee StarsMwenyekiti wa FKF, Sam Nyamweya ameyasema hayo Jumamosi baada ya kukamilisha mazungumzo na mwenyekiti wa CECAFA, ambaye pia ni rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Tanzania, Leodgar Tenga.
Awali FKF, ilikuwa imetangaza kuwa Harambee Stars haitashiriki katika mashindano hayo na badala yake itaaangazia michuano ya kufuzu kwa fainali za wachezaji wanaoshiriki katika ligi za nyumbani barani Afrika CHAN.
Harambee Stars inajiandaa kuchuana na Burundi baadaye mwaka huu.
Wakati huo huo Nyamweya amesema hawataomba mechi hizo za CHAN kuahirishwa na kwamba Harambee Stars itashiriki kikamilifu.
Harambee Stars imepangiwa kucheza mechi yake ya kwanza tarehe Mosi Desemba siku sita tu baada ya kuanza kwa michuano ya CECAFA mjini Kampala na kocha wa Harambee Stars, atalazimika kuwa na vikosi viwili ili kushiriki katika mechi zote.
Malumbano makali yalikuwa yameibuka kati ya viongozi wa soka nchini Kenya na katibu mkuu wa CECAFA, Wycliffe Musonye, baada ya Kenya kutangaza kuwa haitashiriki katika fainali hizo kulalamikia uamuzi wa viongozi wa CECAFA wa kuhamisha mashindano hayo kutoka Nairobi hadi Kampala.