November 07, 2012


Obama Ashinda Muhula wa pili wa Urais 

Hotuba yake ya ushindi
Rais wa Marekani Barack Obama amechaguliwa tena kwa muhula wa pili na kumshinda mpinzani wake wa Republican Mitt Romney.
Barack ambaye ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani, alipata kura 270 za (Electral College) zilizohitajika ili kupata ushindi.
Katika hotuba yake ya ushindi, mbele ya umati mkubwa wa watu mjini Chicago, Obama alisema kuwa atashauriana na bwana Romney kuhusu wanavyoweza kuendesha nchi hiyo.Kura hizi hupigwa na watu maalum wanaoteuliwa na majimbo kulingana na idadi ya miji katika majimbo hayo.
Aidha Obama aliweza kuwashawishi wananchi kumpigia kura na hivyo kushinda licha ya changamoto nyingi zilizowavunja moyo wananchi hususan swala la uchumi.
Obama pia alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mshindani wake Mit Romney.
Wabunge wake wa Democrats waliweza kusalia na idadi yao kubwa katika bunge la Senate ambalo wameshikilia tangu mwaka 2007.
Wabunge wa Republican nao wataendelea kudhibiti bunge la waakilishi, hatua ambayo wadadisi wanasema kuwa huenda likasalia kuwa kikwazo kikubwa kwa Obama na mipango yake ya nchi hasa kuhusu maswala ya sheria.
Sherehe zilizofuata ushindi wa Barack Obama
Katika hotuba yake ya ushindi Obama aliwataka wapinzani wake kushirikiana naye kuleta mageuzi nchini humo.
Zikiwa zimesalia tu kura 29 kutoka kwa jimbo la Florida, Obama aliweza kushinda kura 303 dhidi ya kura 206 za Mit Romney.
Katika kura za ujumla zilizopigwa na wananchi ambazo ni muhimu kisiasa ingawa sizo ambazo zinampa rais ushindi , ushindani mkali ulidhirika kwani Obama alipata asilima hamsini huku Romney akipata asilimia 48.
Obama alimpongeza bwana Romney na mgombea mwenza wake Paul Ryan kwa kuendesha kampeini yao iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Bwana Obama alisema anarejea ikulu ya White house akiwa na motisha zaidi kumaliza kazi aliyoianzisha na kuhakikisha mustakabali mwema kwa wamarekani.
Obama alituma ujumbe kwenye Twitter baada ya kupata taarifa za ushidni wake akiwashukuru wapiga kura
Katika hisia zilizotolewa kote ulimwenguni kufuatia ushindi wa rais Obama, Wizara ya mambo ya nje ya Uchina imesema rais Hu Jintao na waizri mkuu Wen Jiabao wamempongeza Obama kuchaguliwa tena kuwa rais.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, amesema Rais Obama amekuwa kiongozi mwenye mafanikio na alitazamia kuendelea kufanya kazi naye.
Rais wa Umoja wa Ulaya Herman van Rompuy, amesema ana furaha kuhusu ushindi wa rais Obama. Naye waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema uhusiano kati ya nchi yake na Marekani umezidi kuwa na nguvu kushinda siku za nyuma.