Uganda yathibitisha kuwepo kwa Ebola nchini humo
Maafisa afya nchini Uganda wamesema kwamba watu watatu wamekufa baada ya kuugua ugonjwa wa Ebola, lakini serikali haina uhakika kuhusu kilichosababisha visa hivi vilivyotokea Luweero.
Inashukiwa kuwa watu wengine watano wameambukizwa,wawili kati yao wametengwa katika wodi maalum katika hospitali kuu ya Mulago, mjini Kampala.
Hii ni mara ya tano kwa kuzuka kwa Ebola nchini humo katika miaka 12 iliyopita.
Inakadiriwa kuwa watu 17 waliaga dunia magharibi mwa Uganda, kutokana na ugonjwa huo mwezi Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF), hakuna maafa yoyote yaliyoripotiwa kuhusiana na ugonjwa huo hatari tangu mwezi Agosti.
Waziri huyo wa Afya ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa uchunguzi uliofanywa umethibitisha kuwa watu hao waliaga dunia kutokana na ugonjwa huo wa Ebola katika eneo la Luwero, takriban kilomita sitini kutoka mji mkuu Kampala.Watu watano ambao ni wa familia moja wanaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina toka kwa madaktari nchini humo. Wawili kati yao wamelazwa katika chumba maalum katika hospital kuu ya Taifa ya Mulago jijini Kampala.
Hakuna tiba maalum inayojulikana ambayo inaweza kutumika kutibu ugonjwa huo, lakini wagonjwa hupewa dawa za kawaida za kinga pamoja na zile za kupunguza maumivu na kutibu Malaria ili kuongeza kinga mwilini.
Asilimia Tisini ya watu wanaogunduliwa kuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo wa Ebola huaga dunia, na katika kipindi cha miaka Kumi na mbili iliyopita kumekuwa na visa kadhaa vya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda.
Takriban asilimia 50 ya yatu 425 ambao walikuwa wameambukizwa virusi hivyo waliaga dunia mwaka wa 2000.
Wizara ya Afya, pamoja na Shirika la Afya Duniani walikuwa wametangaza kwamba ugonjwa huo ulikuwa haupo tena Uganda. Lakini umezuka tena.
Wanaougua Ebola hupata homa kali, huvuja damu, na viungo vyao vya mwili vya ndani huacha kufanya kazi.
Waganda wengi wanashangaa ni kwa nini nchi yao hukumbwa mara kwa mara, lakini serikali inasema kwamba ni kwa sababu mifumo yao ya uchunguzi imeboreka zaidi.
Hali kadhalika, katika mwezi mmoja uliopita watu tisa wamefariki baada ya kuugua ugonjwa wa homa unaoambukiza wa Marburg, unaofanana na Ebola.