December 29, 2012


WAZALISHAJI WA CHUMVI BAGAMOYO WALALAMIKIA KUPANDA KWA USHURU

WAZALISHAJI wa Chumvi katika Wilaya ya Bagamoyo wamelalamikia ongezeko la ushuru wa chumvi unaodaiwa kupanda kwa asilimia 50 zaidi ya kiwango kilichokuwa kikitozwa hali inayowasababishia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kuliko bei halisi ya masoko.
 
Malalamiko hayo yametolewa mwishoni mwa wiki na Katibu  wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA), Julius Mosha wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa  habari mjini hapa kuhusiana na malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na wadau wa sekta ya chumvi.
 
Mosha alisema kuwa mwaka 2008 Halmashauri hiyo ilipitisha sheria ndogo ya ongezeko la ushuru wa chumvi toka kutoka Sh.50 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh,1000 kwa tani, ikafikia Sh.200 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh.4000 kwa tani, hata hivyo ongezeko hilo lililalamikiwa sana na kudai kuwa inashangaza licha ya kuwa na malalamiko hayo kuna taarifa nyingine ya ongezeko la asilimia 50 zaidi.
 
Alisema licha ya kuwa na malalamiko hayo, Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kufanya maamuzi ya kuongeza ushuru wa aina mbalimbali bila ya kushirikisha wadau kwa mujibu wa sheria hali inayosababisha  kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji kulinganisha na bei ya chumvi katika masoko.
 
Mmoja wa wadau ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) kwa mwaka 2012 anayeongoza kwa kulipa Kodi ya Mapato katika Wilaya ya Bagamoyo Kampuni ya H.J.Stanley and Sons Ltd imelalamikia Wilaya hiyo kutoza ushuru mwingi katika sekta ya chumvi ikiwa ni pamoja na kuwa na urasimu katika baadhi ya mambo yanayohusu uwekezaji.
 
Imeelezwa kuwa licha ya wao kuwa na uzalendo wa kupenda kulipa kodi ya mapato kama sheria inavyowataka kufanya hivyo , lakini wamejikuta wakipambana na ushuru wa Wilaya ambao kimsingi ni mkubwa hali inayowatia wasiwasi katika kuendesha shughuli zao za chumvi.
 
Kauli hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kampuni hiyo Richard Stanley wakati alipokuwa akizungumzia kuongeza kwa ushuru wa chumvi pamoja na changamoto anazokabiliana nazo katika sekta hiyo.