John Terry, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya England, siku ya Jumapili alitangaza kustaafu kama mchezaji wa kimataifa.
Terry, ambaye ni mlinzi wa klabu ya Chelsea, na mwenye umri wa miaka 31, alitangazwa na mahakama ya Westminster mjini London mwezi Julai kwamba hana hatia ya kutumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Anton Ferdinand, tukio ambalo lilifanyika katika mechi ya ligi kuu ya Premier.
Lakini Terry, ambaye alishiriki katika mechi 78 za kimataifa, bado huenda akaadhibiwa na chama cha soka cha FA, kutokana na utovu wa nidhamu, huku chama kikiendelea kusikiliza kesi dhidi yake siku ya Jumatatu.
Alisema: "Kuendelea kufuatia mashtaka dhidi yangu wakati mahakama tayari imeshafanya uamuzi na kupata sina hatia....hayo hayanipi nafasi kutimiza wajibu wangu."
Mwezi Julai mahakama iliamua kwamba Terry hana hatia, lakini wiki mbili baada ya hapo, chama cha FA kilimuandama kwa madai kwamaba alitumia matusi, au maneno yasiyofaa, dhidi ya mlinzi wa QPR, mwezi Oktoba, katika mechi iliyochezwa uwanja uliopo barabara ya Loftus.
Mahakama ilikuwa imesikiliza kesi dhidi ya Terry kuhusiana na madai ya matamshi ya ubaguzi wa rangi, akimuelezea kama "mweusi" na maneno mengine yasiyofaa.
Upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kikamilifu na pasipo na shaka yoyote kwamba Terry alitumia maneno hayo.
Lakini chama cha FA huenda kikamuadhibu kwa kuangalia tu kwamba kulikuwa na uwezekano huo, na hasa ikiwa alimuelezea mchezaji mwenzake kwa njia ambayo iligusia maneno kuhusu asili, au rangi yake.
Terry alimpigia simu meneja wa England, Roy Hodgson, kabla ya kuwasilisha wazi taarifa yake Jumapili jioni.
Terry alimrithi David Beckham kama nahodha mwaka 2006, lakini alivuliwa wadhifa huo mwaka 2010, kufuatia madai kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa zamani wa mchezaji mwenzake katika timu ya England, Wayne Bridge.