UTATA mkubwa umegubika mauaji ya Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza (RPC), Liberatus Barlow ikiwa ni pamoja na utambulisho wa mwanamke aliyekuwa na marehemu kabla na wakati wa tukio hilo na mazingira ya tukio husika.
Marehemu Barlow aliuwawa na kundi la watu wanaosadikika kuwa ni majambazi waliommiminia risasi za moto sehemu mbali mbali za mwili wake, kisha kupoteza maisha papo hapo.
Tukio hilo limetokea kati ya saa 7 na saa 8 usiku wa kuamkia ijumaa, katika maeneo ya Kitangiri karibu na TAI FIVE hoteli barabara ya Kona yaBwiru jijini Mwanza.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Mwanza, Lily Matola, 'mauaji hayo ya kinyama dhidi ya Kamanda Barlow yalitekelezwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, na kwamba walifyatulia risasi maeneo ya shingoni'.
Alisema, ingawa bado hawajafahamu idadi hasa ya risasi zilizosababisha kifo cha RPC huyo, tayari jeshi la polisi limeshaanza kufanya uchunguzi wake mkali na wa kitaalamu zaidi ili kuwakamata watu wote waliohusika katika shambulizi hilo la kinyama.
Taarifa za kutatanisha zimeelezwa kwamba, kabla RPC huyo hajafikwa na mauti alikwenda kushiriki kikao cha harusi ya mtoto wa dada yake aliyetajwa kwa jina la Sembeli Mareto, kilichofanyika Florida hoteli iliyopo maeneo ya Kitangiri, na kwamba kikao hicho cha harusi kilimalizika majira kati ya saa 4-6 usiku. “Ni kweli Kamanda wetu wa Polisi Liberatus Barlo amefariki dunia kwa kupigwa risasi za moto.
Ni tukio kubwa sana na la kinyama!. Haijafahamika alimiminiwa risasi ngapi hadi kufariki dunia papo hapo. “Tayari upelelezi wa kina umeshaanza. Na tutahakikisha watu wote waliohusika katika shambulizi hilo wanakamatwa,” alisema.