Kesi ambayo bingwa wa Olimpiki wa Kenya, Ezekiel Kemboi alishtakiwa kwa kumshambulia Ann Njeri Otieno mjini Eldoret Mkoani Rift Valley mwezi wa Julai mwaka huu, imetupiliwa mbali na mahakama mjini humo
Kulingana na hakimu wa mahakama ya Eldoret Francis Kyambia mlalamishi Njeri amekubali kesi hiyo waimalize nje ya korti.
Lakini kabla ya kesi hiyo kusikilizwa tena, Bi Njeri Otieno aliambia mahakama kuwa alimua kumwodolea mashtaka Kemboi.Anne Njeri Otieno alidai kuwa mwanaridaha huyo alimshambulia alipokataa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye mwishoni mwa mwezi Juni .
Bwana Kemboi, anayefanya kazi katika idara ya polisi daima amekuwa akikanusha madai hayo
Hakimu alimwachilia kwa dhahama ya dola 230 mwanariadha huyo mwishomi mwa mwezi Juni na kumruhusu ashiriki michezo ya Olimpiki mjini London ambako alishinda medali yake ya pili ya dhahabu.
Bi Njeri aliwaambia waandishi wa habari kuwa alifutilia mbali kesi hiyo kwa sababu anataka kuendelea na maisha yake.
Njeri alikuwa amemshtaki Kemboi kwa kumshambulia na kisu nje ya nyumba yao iliyoko mtaa wa West Indies mjini Eldoret akiwa ndani ya gari lake. Lakini Kemboi alidai ni Njeri ndiye aliyemshambulia akiwa na watu wanne.
Hatimaye Kemboi, ambaye hufurahisha mashabiki sana kwa densi yake murwa kila anapoibuka mshindi uwanjani, alisafiri hadi London na timu ya Kenya na kushinda dhahabu mbio za mita elfu tatu kuruka viunzi na maji.