KARIBUNI
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeandaa mkutano na wadau
utakaofanyika Oktoba 9, 2012 saa 04:00 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee.
Lengo la mkutano huu ni kutaka kupata maoni ya moja kwa moja
kutoka kwa wananchi tunaowahudumia kuhusu kuridhika au kutoridhika kwao na
huduma tunayotoa. Wananchi wataeleza ni maeneo gani hawaridhiki nayo na pia
watapata fursa ya kushauri nini kifanyike ili kuboresha huduma za tiba,
uchunguzi, upasuaji n.k
Hospitali inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje wasiopungua 1,000 hadi
1,200 kwa siku na wagonjwa waliolazwa kwa wakati wote wodini ni kati ya 1,000
hadi 1,200 kwa siku.
Hospitali imeonelea ni wakati muafaka wananchi kutumia fursa hii
kushiriki katika mkutano huu kutoa maoni yao moja kwa moja.
Mkutano huu utahudhuriwa na Menejimenti ya Hospitali ikiongozwa na
Mkurugenzi Mtendaji ambayo ndiyo yenye dhamana na kusimamia utendaji wa kila
siku wa Hospitali.
Wakuu wa Idara zote ambazo huduma zinatolewa katika maeneo yao
watakuwepo katika Mkutano huo ili kusikia moja kwa moja kutoka kwa wananchi juu
ya utendaji wa idara zao kwa wananchi wanaowahudumia.
Tunaomba kuchukua fursa hii, kwa dhati kabisa kuwaalika wananchi
kufika na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ili kutoa maoni yao.
Tunaamini kuwa maoni yao ni ya muhimu sana na ndiyo maana tumetoa fursa hii ili
tupate mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wadau tunaowahudumia.
Kama kuna swali lolote ambalo mwananchi angependa kuuliza kabla ya
mkutano huo anaweza kutuma kupitia barua pepe info@mnh.or.tz nasi
tutalifanyia kazi na kutoa majibu siku hiyo hiyo ya mkutano. Aidha unaweza
kutuma maoni yako kwa njia ya posta kwa Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Taifa
Muhimbil, S. L. P. 65000 Dar Es Salaam. Tutaipokea barua yako na tutaijibu.
Ndugu wananchi, tunarudia tena kuwaomba kushiriki kikamilifu
katika mkutano huu ili kutoa maoni yenu juu ya huduma mablimbali zitolewazo na
hospitali ya taifa. Karibuni sana..
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Oktoba 4, 2012