Tanzania na Malawi zazozania nini ?
Ziwa Malawi
Hali ya wasiwasi inatanda kati ya Malawi na Tanzania kuhusu mzozo wa mpakani ambao umekuwa ukitokota kwa miaka mingi lakini sasa umefika daraja ya juu katika wiki chache zilizopita.
Mzozo unahusu umiliki wa ziwa Malawi ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika na ambalo linapakana na Malawi, Tanzania na Msumbiji. Msumbiji haijahusika kivyovyote na mzozo huu.Tangu miaka ya sitini, Tanzania na malawi zimekuwa zikizozana kuhusu umiliki wa ziwa hilo, lakini mzozo huu wa sasa umekuwa mbaya zaidi hasa ikizingatiwa ripoti za kupatikana gesi na mafuta katika ziwa hilo.
Nini hasa kinazozaniwa?
Fahari ya nchi na maswala ya kujiendeleza kiuchumi kwa Malawi na Tanzania kila mmoja akisimama kidete kusisitiza msimamo wake.
Kwa Tanzania, ziwa hilo linajulikana kama Nyasa, wakati nchini Msumbiji inajulikana kama Lago Niassa.
Malawi na Tanzania ni koloni za zamani za Uingereza wakati Msumbiji ilikuwa chini ya ukoloni wa Ureno. Uingereza iliichukua Tanzania kutoka kwa Wajerumani baada ya wao kushindwa katika vita vya kwanza vya dunia.
Kando na ripoti za kuwepo mafuta na gesi katika ziwa hilo, ziwa lenyewe ni kivutio kikubwa cha watalii.
Malawi inasema inashauriana na Msumbiji kuhusiana na uchimbaji wa mafuta katika siku za baadaye ili kuzuia mzozo wa kidiplomasia .
Je hii ni mara ya kwanza kwa mzozo huu wa ziwa Malawi kutokea?
Hapana. Mapema miaka ya sitini, Malawi ilidai umiliki wa ziwa hilo kwa kuambatana na makubaliano ya mwaka 1890 Heligoland kati ya Uingereza na Ujerumani ambayo yalisema kuwa mpaka kati ya nchi hizo uko upande wa Tanzania.
Makubaliano hayo yaliafikiwa na Muungano wa Afrika na Tanzania ikaitikia ingawa shingo upande. Mzozo mpya kati ya nchi hizo ukaripotiwa tena kati ya mwaka 1967 na 1968.
Nini chanzo cha mzozo huu wa hivi sasa?
Mwezi Septemba mwaka 2011, Malawi ilitoa leseni ya kuchimba mafuta kwa kampuni ya British Surestream Petroleum Limited. Sehemu iliyotolewa kwa uchimbaji wa mafuta ni sehemu yenye mraba wa kilomita 20,000 sehemu ambayo Tanzania inasema ni yake.
Vyombo va habari viliripoti mwezi Julai kuwa , mitumbwi ya wavuvi na ya watalii kutoka Malawi inavuka na kuingia upande wa Tanzania
Tanzania nayo ikasema kuwa itatafuta ushauri kutoka jamii ya kimataifa ikiwa nchi hizo hazitaweza kusuluhisha mzozo huo zenyewe.
Nchi hizo mbili zilifanya mkutano mwezi Julai mjini Dar es Salaam kuhusu mzozo wa mpaka
Tarehe 30 mwezi Julai, Tanzania, iliitaka Malawi kusitisha shughuli za kutafuta mafuta kwenye ziwa hilo hadi mzozo kati yao utakaposuluhishwa lakini maafisa wa Malawi wakasisitiza kuwa ziwa hilo lote ni la Malawi na kwamba hakuna sababu ya kusitisha shughuli zake za kutafuta mafuta
Tanzania ilisema kuwa ikiwa Malawi itaendelea na shughuli zake kutafuta mafuta itaathiri mazungumzo yanayoendelea kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe alisema kuwa ikiwa Malawi haitafuata maagizo hayo, Tanzania itaiona hatua yake kama kitendo cha uvamizi.
Nini kimesababisha hofu ya hatua za kijeshi?
Hofu ya mzozo kutokota na kuwa mbaya zaidi ilijitokeza wakati Tanzania iliposema kuwa italinda mipaka yake na kuzingatia sheria za kimataifa.
Maafisa kutoka pande zote walikutana tena mjini Dar es tarehe 4 na 5 mwezi Agosti, lakini Malawi ilisisitiza kuwa haitasitisha shughuli zake za kutafuta mafuta
Waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania Membe alinukuliwa akisema katika taarifa yake kali kuwa watapambana na Malawi kijeshi.
Matamshi yake aliyatoa bungeni kulingana na taarifa kwenye mtandao wa The Guardian.
Mtandao wa Nyasa Times ulitoa taarifa kuonyesha kuwa kuna taharuki kati ya nchi hizo mbili kuhusu mpaka wa Ziwa , lakini waziri wa usalama wa ndani wa Malawi Uladi Mussa akasisitiza utulivu.
"Tunashauriana na serikali ya Tanzania na mambo yatakuwa sawa. Ikiwa hali itakuwa mbaya kesi hii tutaiwasilisha kwa mahakama ya kimataifa ya haki" alisema waziri huyo.
Mnamo tarehe 11 mwezi Agosti, Rais wa Malawi Joyce Banda alisema kuwa yuko tayari kufanya kila hali ikiwemo kujitolea maisha yake kwa sababu ya watu wa Malawi.
Watanzania wanaoishi karibu na ziwa hilo wakaanza kutoroka wakihofia vita.
Je kumekuwa na juhudi za kidiplomasia kumaliza mzozo huu?
Maafisa wa chi hizi mbili walikutana kati ya tarahe 20 na 25 mwezi Agosti, mjini Mzuzu,Kaskazini mwa Malawi, lakini Rais Banda akarejelea msimamo wake kuwa ni wazi kuwa Ziwa hilo ni la Malawi.
Wakati wa mkutano wa chi za ukanda wa Afrika Kusini (SADC),nchini Msumbiji, Rais Banda alikutana na mwenzake wa Tanzania Jakaya Kikwete, aliyekana kuwa nchi yake inajiandaa kwenda vitani na Malawi. Kikwete alisema kuwa matamshi kuhusu vita yalitolewa na wanasiasa wa upinzani ambao wana jazba.
Mjini Mzuzu mkutano uliisha bila maafikano. Siku chache baadye Rais Banda alisema kuwa mzozo huo utasuluhishwa katika mahakama ya kimataifa ya ICJ.
Malawi baadaye ilikosa kufika kwenye mkutano kati yake na Tanzania kati ya tarehe 10 na 15 Oktoba kulingana na mtandao wa The Citizen
Je Juhudi za kidipmomasia zimefanikiwa?
Hapana. Mwanzo Tanzania imepandisha mzozo huo kwenye daraja ya juu zaidi kwa kutoa ramani mpya inayoonyesha mpaka ulio katikati mwa ziwa Nyasa.
Afisaa mmoja kutoka wizara ya nyumba wa Tanzania amesema kuwa ramani hiyo inaondoa hali ya kutoelewana kwa kuonyesha mpaka unaozozaniwa.
Tarehe tatu mwezi Oktoba Rais Joyce Banda aliakhirisha mkutano kati ya nchi hizo mbili hadi Tanzania itakapojieleza kuhusu ramani hiyo.
Alimtuhumu Rais Kikwete kwa kumhadaa na kwamba anapanga kulipua mitumbwi ya Malawi katika ziwa hilo.
Kikwete alitangaza siku hiyo hiyo kuwa Tanzania itawasilisha kesi yake katika mahakama ya kimataifa ya mizozo.
Kwa upande wake Rais Banda ameutaka muungano wa Afrika kuingilia kati mozo huo.
Je mzozo huu ni kuhusu mpaka tu au kuna jengine?
Habari na : Bbc