200 wajeruhiwa wakitafuta Ajira nchini Tunisia
Mmoja wa waliojeruhiwa wakitafuta ajira huko Tunisia
Zaidi ya watu mia mbili walijeruhiwa huko Tunisia Jumatano katika siku ya pili ya maandamano jijini Siliana kilomita mia moja Ishirini kutoka katika jiji kuu la Tunis.
Waandamanaji hao walikuwa wakimtaka gavana wa eneo hilo kujiuzulu, kutaka msaada wa kiuchumi na vile vile kushinikiza watu kumi na wanne waliokamatwa katika ghasia za Aprili kuachiliwa.
Vyama vya wafanyakazi vimeitisha maandamano zaidi baadaye leo.Maafisa wa usalama walitumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira kuwatwanya watu waliokuwa wanataka ajira. Pia kulikuwa na ripoti za watu kutibiwa baada ya kupata majeraha ya risasi.
Tunisia ndiyo ilikuwa kitovu cha mapinduzi ya kiraia katika nchi za Kiarabu ambapo wananchi walimng'oa mamlakani rais wao wa muda mrefu Januari mwaka 2011.
Kususia chakula
Waziri mkuu wa nchi hiyo Hamadi Jebali amekataa wito wa waandamanaji kuwa aondoke mamlakani akisema kupitia televisheni kuwa Gavana hang'atuki
Mwandishi wa BBC Sihem Hassaini ambaye yuko mjini Tunis, anasema kuwa maandamano hayo ni ya hivi karibuni katika msururu wa maandamano mengine ya watu wanaeolezea kukerwa na ukosefu wa mageuzi ya kuridhisha tangu mapinduzi ya kiraia kufanyika.