November 23, 2012


Athari Za Boko Haram Huko Nigeria

Mkutano wa wakristo waliopoteza makao yao kufuatia ghasia Nigeria
Kundi la kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria, na vikosi vya usalama, wote wametuhumiwa na shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International kwa kufanya vitendo vya kukiuka haki za binadamu hasa katika eneo la Kaskazini lenye waisilamu wengi nchini Nigeria.
Boko Haram, ambalo jina lake linamaanisha elimu ya kimagharibi imeharamishwa, kufanya harakati za kuiangusha serikali na kuunda taifa la kiislamu !.
Hivi karibuni siku ya Jumapili, kanisa lilishambuliwa na kusababisha vifo vya watu wanane mjini Kaduna, mojawapo ya miji ambayo imeathirika kutokana na mzozo unaoendelea kati ya serikali na Boko Haram.
Ingawa hawajakiri kufanya mashambulizi hayo, kundi hilo limewajibika wakati lilipofanya mashambulizi Kaskazini na kati kati mwa Nigeria.
Obadiah Diji, kiongozi mmoja wa vijana wa kikristo mjini Kaduna, alisimulia BBC ambavyo maisha yamebadilika mjini humo.
“ watu wanaogopa hata kutoka nje usiku au hata kukaa nje tu kunywa pombe au hata kula samaki."
"Nimeishi mjini Kaduna karibu maisha yangu yote na nimejawa na huzuni sana nikiona ambavyo mji huu umegawanyika sana kwa ,misingi ya kidini."
"Waislamu wanaishi ambako idadi yao ni kubwa, wakristo nao vile vile. Kwa hivyo makundi hayo mawili ya watu, yanaishi maisha yao kivyao bila kutangamana"
"Sio kawaida kuwa hivi. Wakati mmoja tulijivunia kwa sababu ya umoja uliokuwa unadhihirika hapa Kaduna na kila mtu alikuwa anakaribishwa hapa."
                                 Wanigeria wakifanya maombi
"Ingawa kulikuwa na migawanyiko, wakristo na waislamu waliishi kwa pamoja. Tulikuwa tunatembeleana . Watoto wetu walisoma katika shule moja , wakijifunza kutoka kwa kila mmoja kuhusu dini na tamaduni zao."
"Watu hata walioana licha ya dini zao mfano mamangu wa kambo alibadili dini na kuwa muislamu na kisha akaoa muislamu pia."
"Dada yangu pia aliolewa na muislamu ingawa alisalia kuwa mkristo tu ."
Kwa simulizi hii ya Obadiah Diji kutoka Kaduna tunagundua kwamba kuna ndoa nyingi kama hizo mjini Kaduna ingawa mfumo huo haukuwahi kusababisha matatizo yoyote hapo awali . Watu waliheshimiana na kustahimiliana bila chuki na ghasia kama ilivyo sasa .
Kwa mujibu wa Obadiah Diji,hali ya chuki na ghasia ilianza kulipotiwa tangu mwaka 2000 wakati Kaduna iliposhambuliwa kwa mara ya kwanza na mzozo wa kidini ambao unachochewa na makundi yanayotaka sheria za kiislamu.
Hapo ndipo makundi yaliyohisi kutengwa yalijitokeza. Watu walitoroka makwao kwa sababu ya ghasia. Wakristo walijikuta wakiishi katika eneo lao mjini kaduna huku waislamu nao wakiwa wakiishi maeneo yao !!.
Amekuwa akipinga maeneo yaliyotengewa jamii moja na ndiyo maana bado anaishi na mkewe na watoto wake wanne katika eneo ambalo ni la waislamu wengi.
Wanawake katika mikutano kadhaa maeneo ya Kaskazini wamepigwa marufuku kubeba vibeti kanisani. Makanisa mengi sasa yana vifaa vya kuwachungua watu wanaoingia kanisani ikiwa wana silaha yoyote au la.
Wanawake wanazuiwa kubeba vibeti kwa sababu mshambuliaji anaweza kuingia kanisani akiwahadaa watu kuwa ni muumini kumbe amebeba silaha kwenye kibeti [mkoba]  chake.
Kwa hivyo maisha yao ya kidini yameathiriwa sana, na hata maisha ya kijamii.
Sasa wanaishi maisha ya faragha muda wote wakikaa nyumbani kipweke !!. Ni polisi pekee ambao wanaonekana barabarani usiku wakiwa katika dolia zao.
Hata hivyo ghasia zimewafanya watu wengi kuwa na imani sana juu ya maisha ya kupambana na maadui wakati wote .
Wakristo wengi wanaoishi katika ugumu huu hujenga imani ya kuishi kwa Imani Kuu Ya Kuamini Kitabu Cha Biblia ambacho kinasema kuwa Mtu atapita Katika Mateso na Ugumu Wa Maisha kama alivyoteswa Bwana Yesu Kristo Wakati wa Uhai Wake.
Hata hivyo nia ya Maisha kwa Binadamu Duniani kote ni kuhakikisha Kila Binadamu anapata haki ya kuishi bila kujali itikadi za dini, kabila, rangi au muonekano wake katika jamii zetu zote Duniani kote.
Jambo la kujivunia ni kwamba Wakristo na Wasilamu nchini humo husoma kwa pamoja ili kuandaa Taifa imara  kwa mustakabali wa nchi hiyo kwa sasa na baadae.
Ni matumai yetu kuwa kizazi cha sasa na kijacho nchini humo ndiyo chachu ya mustakabali wa maendeleo endelevu kwa  nchi hiyo yenye nguvu kijeshi, kisiasa, kiuchumi na hata iliyojengeka kwa sifa ya kuwa na idadi kubwa ya kizazi cha wasomi wengi wa elimu ya juu kulinganisha na mataifa mengi ya Afrika.
Mfumo wa kisasa wa maisha umesababisha athari kuliko manufaa.