November 20, 2012


Waasi wa M23 waendeleza mashambulizi ya kijeshi kuingia mjini Goma - DRC

Watu wakikimbia mapigano Goma
         Watu wakikimbia mapigano Goma
Wapiganaji wa waasi wa M23, hatimaye wamefanikiwa kuingia mji mkuu wa eneo la Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mwandishi wa BBC mjini Goma anasema wapiganaji hao wa waasi walikabiliana kwa risasi na wanajeshi wa serikali, ambao walitoroka baada ya kuzidiwa nguvu.
Jeshi la Umoja wa Matifa la Kutunza amani katika eneo hilo limekanusha madai kuwa wapiganaji hao wa waasi wanathibiti uwanja wa NDEGE.
Maelfu ya watu wametoroka makwao kufuatia mapigano hayo, ambayo yamezua wasi wasi wa kuzuka upya kwa mapigano nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mapigano ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu milioni tano.
Hii ni mara ya kwanza tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003, ambapo wanajeshi wa waasi wamefanikiwa kuingia mji huo wa Goma.
Takriban watu nusu milioni wanakadiriwa wanaishi mjini humo.

Serikali ya Rwanda imekanusha madai ya mara kwa mara kutoka kwa serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa inawaunga mkono wapiganaji hao wa waasi wa M23.
Awali serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilipuuzilia mbali makataa iliyotolewa na wapiganaji wa waasi wa kuanzisha mazungumzo ya amani, na kukariri kuwa itaendelea kuilinbda mji wa Goma, Mashariki mwa nchi hiyo.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa umelaaini hatua hiyo ya waasi wa M23 ya kuendelea na mapigano huku wakielekea mji wa Goma.
Mapigano hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi tangu mwezi Julai Mwaka huu katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.