Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zimekubaliana kukutana na mdhamini mMkuu wa Ligi hiyo (Kampuni ya Simu za Mkononi - Vodacom) ili kuzungumzia kipengele cha mkataba wa ligi hiyo kinachozuia kampuni nyingine za mawasiliano kudhamini timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
Katika kikao kati ya Viongozi wa Vilabu na Kamati ya Ligi kilichofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wallace Karia, na kupitisha maazimio hayo.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
Maazimio mengine ya kikao hicho ni TFF kuiandikia barua African Lyon ambayo itaipeleka kwa mdhamini wake (Zantel) ikielezea hatua hiyo ili kusimamisha udhamini huo wakati ikisubiri matokeo ya mazungumzo kati ya klabu hizo na mdhamini wa Ligi Kuu juu ya kipengele cha kuzuia washindani wa Vodacom.
Katika mkutano huo, watendaji wawili wa Kamati ya Ligi ambayo iko katika kipindi cha mpito kuelekea kuundwa kwa Bodi ya Ligi walitambulishwa kwa klabu hizo. Watendaji hao ni Silas Mwakibinga ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Joel Balisidya ambaye ni Ofisa wa Ligi (LO).
Boniface Wambura
Afisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)