Mbinu Mpya na Nafuu ya Kupima HIV.
Aina na mbinu mpya ya kuchunguza na kuona viwango vidogo kabisa vya virusi na hata aina ya saratani, imezinduliwa na watafiti nchini Uingereza.
Utafiti huo unahusu majimaji ambayo hubadilika rangi kuonyesha kuwa mtu ameathirika au hapana.
Aidha watafiti wamesema mbinu hii mpya ambayo inahitaji utafiti zaidi, inaweza kuelezea kwa kina aina ya ugonjwa au virusi mfano proteni inayopatikana kwenye kirusi cha HIV.
Watafiti wa uchunguzi huo kutoka chuo kimoja kikuu mjini London, wanasema kuwa mbinu hiyo inaweza kuchangia kuhamasisha watu kupimwa Virusi vya HIV na magonjwa mengine kwani njia zingine za kupima maradhi hayo bado ni ghali.
Ikiwa dalili ya kirusi au ugonjwa ipo katika matokeo ya uchunguzi, basi inabadili rangi ya kemikali. Matokeo yatakuwa rangi ya bluu, na ikiwa kirusi kipo na nyekundu ikiwa kirusi au ugonjwa haupo.
Watafiti wanasema kuwa matokeo ya uchunguzu au upimaji pia yatapatikana kwa haraka zaidi.
Profesa Molly Stevens aliambia BBC:
" Mbinu hii ya kupima magonjwa inatumiwa kuchunguzwa virusi hata kama ni vya viwango vya chini mno na kuongeza nafasi ya kuona kama ugonjwa upo kwenye mwili wa mtu au hapana."
"Kwa mfano, ni muhimu kuchunguza viini vya ugonjwa vilivyo na viwango vya chini sana vya mfano saratani kwa mtu aliwahi kutibiwa ugonjwa huo kuona ikiwa saratani hiyo itaweza kuibuka tena hata baada ya kutibiwa, pia inaweza kusaidia katika kupima wagonjwa wa HIV, ambao viwango vya virusi viko chini sana kiasi cha kutoweza kuonekana kwa mbinu za sasa."
Watu waliopimwa mapema kutumia mbinu hii ya rangi, walionyesha dalili za HIV na saratani ya tezi ya kibofu, ingawa utafiti wake katika nyanja za juu bado utahitajika kabla ya kutumika hospitalini.
Watafiti wanasema kuwa wanatarajia kuwa gharama ya kifaa hicho itakuwa ndogo mara kumi kuliko mbinu za sasa za kupima magonjwa na kwamba itanufaisha watu katika nchi ambazo mbinu zilizopo hawawezi kuzimudu. Na pia itaweza kutumika sana katika kupima virusi vya HIV katika nchi maskini duniani.