Kampuni inayochimba dhahabu nyeupe nyingi kabisa duniani, ya Anglo American Platinum, imekubali kuwarejesha makazini wachimba migodi zaidi ya 12,000 wa Afrika Kusini iliowasimamisha kazi kwa sababu kutekeleza mgomo kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo imekubali kuwapokea wachimba migodi hao baada ya mgogoro mkubwa wa wafanyakazi hao kuhusiana na maslahi yao kazini.
Hata hivyo habari za kuaminika kutoka Chama cha wachimba migodi, NUM, zimesema kuwa kampuni hiyo imekubali kuwapokea wachimba migodi hao iwapo watarudi wenyewe kazini ifikapo Jumanne ya wiki ijayo.
Sekta ya migodi nchini Afrika Kusini ilikumbwa na migomo kadha ambayo serikali inasema imeigharimu nchi hiyo zaidi ya dola bilioni moja hadi sasa !.
Watu kadha wameuwawa kwenye ghasia zilizohusisha migomo hiyo katika sekta ya madini nchini humo.